Karibu Dj Dukeswagas blog

Sunday, February 26, 2017

NINATARAJIA KUIBORESHA BLOG HII

BLOG hii imekuwa kimya kwa muda mrefu sasa lakini ninamatarajio ya kuiboresha je mdadhani kwa hali ya speed ya mtandao kwa maeneo uliyopo inaweza kutusaidi kukufikishia habari na kufunguka kiurahisi hebu nifahamisheni .asante

Tuesday, November 4, 2014

Ray C wa kiuno bila mfupa abadilika

Ray C wa kiuno bila mfupa abadilika

Mwanamuziki wa siku nyingi, Ray C.PICHA|MAKTABA 



Mwanamuziki wa siku nyingi, Ray C ametangaza kuwa atatoka mwezi huu, lakini akiwajulisha mashabiki wake kuwa safari hii ataweka nguvu zaidi kwenye uimbaji badala ya unenguaji, ambao ulimpa umaarufu.
Ray C, ambaye ametamba kurudi rasmi na kibao cha “Mshum Mshum”, amesema ingawa mashabiki wake walimzoea kwa umahiri wake katika kukata viuno, sasa watarajio vitu tofauti; muziki anaoufanya ni ule wa kuonyesha kipaji chake cha kuimba.
Akizungumza na Mwananchi, Ray C alisema mwezi huu anatarajia kurudi rasmi katika anga za muziki kwani ameshahakikisha kuwa harakati zake za kupambana na dawa za kulevya kupitia mfuko wake wa Ray C Foundation, zimesimama imara hivyo ni wakati wa kurudi ili aendelee na kampeni yake upande wa pili.
“Ninatarajia kuachia nyimbo zangu mpya za “Kiss Kiss” au “Mshum Mshum” mwezi huu, lakini mashabiki wangu wajue kwamba safari hii ni kuonyesha kipaji cha kuimba, hakuna mambo ya kiuno bila mfupa, nimebadilika kwa kiasi kikubwa sana,” alisema.
Ni kitambo toka Ray C, ambaye jina lake halisi ni Rehema Chalamila, kuonekana kwenye muziki baada ya ukimya wa muda mrefu uliotokana na matatizo ya utumiaji wa dawa za kulevya, ambao anakiri ulimrudisha nyuma kimaisha.
“Natamani wasanii wengine wasiguse kabisa hii kitu. Binafsi imenirudisha nyuma sana. Kwa sasa nimesharekodi studio za Legendary Music Studio kwa Tudd Thomas na kwingineko,” alisema.
Ray C alizidi kufunguka kwa kudai kuwa ujio wake mpya pia utahusisha nyimbo za taarabu.
“Albamu yangu ambayo inakuja hivi karibuni ina mchanyiko wa nyimbo mbalimbali, zikiwemo taarab na za kihindi. Nimefanya taarab kama mbili na zook, yani nimebadilika kabisa,” alisema.
kuna kwaito, kuna bongoflava,uhindi hindi kidogo,” alisema Ray C.

Chanzo mwananchi 


Wednesday, May 7, 2014

Ugonjwa wa homa ya dengue umefikia hatua mbaya.


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid.PICHA|MAKTABA


Dar es Salaam. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa tamko kuwa ugonjwa wa homa ya dengue umefikia hatua mbaya.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema jana kuwa kuna hali ya hatari na maambukizi ya ugonjwa huo yanaongezeka, hivyo wananchi wanatakiwa kuwa makini.
“Kwa ufupi, mbu sasa ni hatari kuliko ilivyokuwa awali kwa sababu hawa wanaoambukiza homa ya dengue huuma wakati wa mchana, tofauti na wale wanaoambukiza malaria ambao huuma usiku na watu walikwishajua kujikinga kwa chandarua au dawa,” alisema.
Waziri Rashid aliwataka wananchi kuchukua hadhari kwa sababu ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba... “Kila mtu anatakiwa kuchukua hatua, maji yasiruhusiwe kutuama kwa muda mrefu kwani humo ndimo mbu huzaliana kwa wingi. Kwa mfano, maji yanayotuama kwenye kofia za mabati, kwenye vifuu na kwenye madimbwi yanatakiwa yaondolewe ili kuzuia mbu hao.”
Alisema ni vyema watu waende hospitali kupima badala ya kuuchukulia kila ugonjwa kuwa ni malaria na akawataka wasipende kutumia dawa kwa matakwa yao kabla ya kuonana na daktari.
Daktari Mtafiti katika Kliniki ya Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Belia Klaassen alisema tangu Januari mwaka huu hadi jana, watu waliogundulika kuambukizwa dengue ni 203, kati yao 110 waliugua Aprili pekee.
Alisema tatizo hilo linaongezeka kwa kuwa kuna wagonjwa 20 wapya wanaogundulika kila siku.
NIMR kufanya utafiti
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti cha Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Julius Massaga alisema: “Upo uwezekano wa kufanya utafiti wa tiba ya ugonjwa huo. Kwa ufupi, huyo mbu anayesababisha homa ya dengue yupo hata hapa kwetu NIMR, kwenye mazingira yetu.”
Dengue ilianzia IFM
Tukio la kwanza katika mfululizo kugundulika kwa maradhi hayo lilibainika miaka mitatu iliyopita baada ya wanafunzi kadhaa wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kufariki dunia mfululizo.
Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Mwananyamala, Mrisho Rupinda alisema jana kwamba wagonjwa hao walibainika mwishoni mwa 2011 na baada ya uchunguzi wa awali ilibainika kuwa idadi kubwa waliathiriwa na dengue.

Chanzo: gazeti Mwananchi